Thursday, June 19, 2014

Unajua jinsi gani watu waishio maeneo ya karibu ya Mlima Kilimanjaro wanatunza mlima Kilimanjaro?

 
Wananchi wanaoishi maeneo ya kuzunguka mlima Kilimanjaro wametakiwa kupanda miti kwa wingi katika maeneo yao, ili kuweza kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo yameyakumba maeneo mbalimbali hapa nchini na kusababisha madhara makubwa ikiwemo ukame wa kipindi kirefu.

Rai hiyo ilitolewa na mwenyekiti wa taasisi inayojishughulisha na utunzaji wa mazingira kwa vitendo mkoani Kilimanjaro (TEACA), Adoncome Mcharo, wakati wa zoezi la upandaji wa miti katika eneo la nusu maili lililoko katika kijiji cha ruwa kata ya kilema kaskazini, wilaya Moshi mkoani Kilimanjaro. 

Mcharo alisema kuwa maeneo mengi ya vijiji vinavyozunguka mlima Kilimanjaro yameathiriwa kwa kiasi kikubwa na uharibifu wa mazingira unaofanywa na baadhi ya watu kwa kukata miti hovyo, uchomaji moto mlima, hali ambayo imesababisha barafu ya mlima huo kupungua kwa kiasi kikubwa.

Alisema Teaca kwa kushirikiana na kamati za mazingira, wananchi na viongozi wamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha  wanapanda miti ili kuweza kurudisha uoto wake wa asili ambao ulikuwepo hapo awali.

Mwenyekiti huyo alisema zoezi hilo ni endelevu na linatokana na mpango walioufanywa tangu mwaka 2010/2011 ambapo walifanikiwa kupanda miti elfu kumi katika maeneo yote yanayozunguka mlima Kilimanjaro, ambapo kwa kipindi cha mwaka 2012/2013 wamejiwekea lengo la kupanda miti zaidi ya elfu kumi na tano katika maeneo hayo.

Aidha Mwenyekiti huyo aliitaka Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa), kuacha kutumia silaha mbalimbali kuwafukuza wananchi, kwa kuwa wananchi hao ndio wamekuwa mstari wa mbele katika upandaji na utunzaji wa miti na mazingira hayo, hivyo kinachopaswa kufanywa na hifadhi hiyo ni kujenga uhusiano mzuri na wananchi hao.

Nao baadhi ya wananchi wanaozunguka maeneo hayo, wameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuwaruhusu  kuingia kwenye  maeneo ya nusu maili ili kuweze kukata majani kwa ajili ya mifugo kutokana na kwamba wakati wa kampeni ya upandaji miti wao ndio wamekuwa wahusika wakubwa wa upandaji miti.